Dedicated to creating a peaceful future for elephants in Southern Tanzania, and beyond

Tafiti mpya inayodhihirisha ni kwa sababu gani tembo wanakula mazao

 

Maria Mbata, Frank Lihwa na Josephine Smit

Lengo muhimu la uhifadhi ni kujaribu kuhakikisha kuwa binadamu na wanyamapori wanaweza kuishi pamoja. Hii ni muhimu wakati unapokuja kuwazungumzia tembo, ambao kihistoria wanaishi na wanasafiri nje ya mazingira ya uhifadhi.

Moja ya changamoto ya mshikamano baina ya binadamu na tembo ni uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo. Hali hii inatishia maisha, usalama wa chakula na ustawi wa jamii inayoishi maeneo ya vijijini. Tembo wanapotembelea ndani ya mashamba, wakati mwingine huuwawa kama kisasi au kuuliwa na askari wa wanyama pori chini ya kifungu cha sheria ya wanyama waharibifu. (“Problem Animal Control”). Hali hii hupelekea kudidimizwa kwa jitihada za uhifadhi wa tembo.

Ili tembo na binadamu waweze kuishi pamoja kwa muda mrefu, ni muhimu kutafuta njia za kupunguza madhara ya tembo kwenye maisha ya binadamu na uchumi. Kutafuta njia sahihi, tunahitaji kuelewa kwanini tembo wanakula mazao ya binadamu kuliko chakula cha mwitu, na kwa jinsi gani wanajifunza kuhusu mazao kama chanzo cha chakula.

Kuchunguza maswali haya timu yetu ya Southern Tanzania Elephant Program tulitumia kamera ili kurekodi misafara ya tembo kwenye mashamba. Kamera ziliwekwa maeneo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Tanzania kati ya mwaka 2010 na 2014.

Tuliweka kamera kwenye njia za tembo kando kando ya Hifadhi ya Taifa kurekodi picha za tembo wakati wanasafiri ndani na nje ya mashamba yaliyoko jirani. Pia tulitumia picha zilizopigwa ili kumuainisha kila tembo kwenye vipengele muhimu vinavyo watofautisha kama vile masikio na meno.

Hatari kubwa, Faida kubwa

Tembo wote waliorekodiwa na kamera zetu walikuwa ni madume. Hii inafanana na tafiti za awali zilizo onyesha kwamba kula mazao ni tabia ambayo ni hatari kubwa lakini pia inaleta faida kubwa kwa madume. Sehemu nyingine, majike pia wamerekodiwa kula mazao, lakini kwa ujumla hutembelea mashamba kwa kuhofia hatari iliyopo juu ya watoto wao.

Umri pia una nafasi yake. Utafiti wetu, pamoja na uchunguzi wa awali uliofanyika huko Amboseli, Kenya na Kibale, Uganda, unaonyesha kwamba ulaji wa mazao unahusiana na hatua maalumu kwenye maisha ya tembo dume.

Hatua mbili muhimu zilionekana: mwanzo wa uzalishaji kwa madume huanza wanapofikia umri kati ya miaka 20-30, na kilele cha uzalishaji pale wanapofikia miaka 40. Wakati ambao madume hufikia hatua hizi, huwa wapo tayari kuhatarisha maisha yao na wanakuwa na uhitaji mkubwa wa chakula. Mazao ya binadamu huwa kivutio cha chakula kwa tembo ambao hutaka kuongeza ukubwa wa miili yao na ufanisi katika kuzaliana .

Ni namna gani madume hujifunza kuhusu mazao kama chanzo cha chakula? Tuligundua kwamba madume wadogo wenye umri kuanzia miaka 10-14 walitembelea mashamba. Huu ni umri ambapo dume hutengana na makundi ya familia ya mama zao, kwahiyo hugundua mashamba wakati wa misafara hiyo. Pia iligundulika kwamba dume wadogo hujifunza kuhusu mazao kutoka kwa tembo dume wakubwa. Watafiti huko Amboseli waligundua kwamba ndani ya kundi lenye tembo mzee ambae ni mtumiaji wa mazao, na ana urafiki na dume mdogo ndani ya kundi, kuna uwezekano wa yule dume mdogo kuiga tabia za tembo mzee.

Tembo wangapi wanakula mazao?

Tafiti zingine zimejaribu kugundua madume wangapi wanakula mazao, na jinsi gani tabia za ulaji zinavyo tofautiana. Kwa Udzungwa tuliainisha tembo 48 tofauti kutoka kwenye picha za kamera. Tuligundua kwamba ni madume wengi wanaotembelea mashamba kwenye eneo la utafiti. Kwa hiyo, hatukuweza kusema ni tembo wachache wanaosababisha uharibifu wa mazao.

Vilevile tuligundua kwamba idadi ya misafara ilitofautiana kati ya dume mmoja na mwingine. Theluthi mbili walionekana mara moja ndani ya miaka minne ya muda wa utafiti, hali hiyo inaonyesha kwamba dume hawa walitembelea mashamba mara chache. Theluthi moja ya madume walionekana zaidi ya mara moja, hali hiyo inaonyesha kwamba dume hawa walitembelea mashamba mara nyingi zaidi. Lakini miongoni mwao, walitofautiana kiasi cha misafara kwenye maeneo ya mashamba.

Kwa kulinganisha na nchini Kenya, watafiti walikadiria kwamba 12% ya madume wa Amboseli na 21% ya madume kutoka eneo kubwa la Amboseli, Kilimanjaro na Tsavo-Chyulu walikuwa wanarudia kula mazao. Pamoja na shuhuda hizi zinadhihirisha kwamba madume wengi hula mazao mara chache, wakati idadi ndogo wanaweza kula mazao mara nyingi zaidi.

Mikakati dhidi ya uharibifu wa mazao

Mikakati ya kupunguza upotevu wa mazao unaosababishwa na tembo inatakiwa kuzingatia kuwa madume wengi hula mazao mara chache. Kwa hiyo kuua tembo ambaye anakula mazao haitakuwa suluhisho la tatizo la uharibifu wa mazao. Kuchukua hatua ya kuwaua tembo pia inaweza kuathiri idadi ya Tembo, kwa sababu inawakumba zaidi madume wazee ambao inawezekana wakawa wanakula mazao. Kuwaua madume wazee inaondoa chanzo muhimu cha ujuzi wa ikolojia pamoja na umuhimu wa kila mmoja katika uzalishaji. Hasa itaathiri idadi ya tembo ambao tayari ni tishio kutokana na ujangili wa meno ya tembo.

Kuna njia nzuri zaidi ambazo sio hatarishi za kupunguza uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo. Njia hizi ni fensi za mizinga ya nyuki na matumizi bora ya ardhi. Mbinu hizi zinahitaji nguvu ya kujitoa, jamii yenyewe kukubali, pamoja na ubunifu. Lakini kama tulivyogundua katika kazi zetu maeneo ya kusini mwa Tanzania, njia hizi zinaonyesha tija siku za usoni kwa kuongeza uwezekano wa wakulima na tembo kuishi pamoja.

 

Fensi za mizinga ya nyuki inasaidia kuzuia tembo wasiingie shambani. Pia wakulima wanafaidika na uuzaji wa asali.